KURASA

Ijumaa, 20 Juni 2025

Mada ya Ushuhuda, Uliyochimbuko la Kitabu hiki chaJifunze Kumuamini Roho Mtakatifu Katika Eneo Hilo ...

 Mada ya Kwanza Katika Kitabu Chetu Kipya cha Jifunze Kumuamini Roho Mtakatifu Katika Eneo Hilo...

Na Mwl. Oscar Samba 

 1.Ushuhuda

Chimbiko kuu la kitabu hiki ni tukio binafsi lililonikuta, ambalo moja kwa moja Roho Mtakatifu alilitumia kama somo ili kunivusha mahali lakini pia kwa nia ya kupangua baadhi ya mienendo isiyo sahihi katika njia zangu. Iwe ni za kihuduma au kimaisha kama vile uchumi, kijamii na kadhalika.

Somo hili nimelipata katika mradi ninaoufanya wa kutotolesha vifaranga vya kuku na ufugaji. Siku ya 21 ilipofika, vifaranga vikaanza kuanguliwa; kikanuni ni hadi kitoke kwenye kasha lake, kikauke ndipo ukitoe kwenye mashine.

Mimi vilipoanza tu kutoboa kasha, (eneo la kichwa) nililazimisha kumenya kasha zima. Hali iliyovipelekea kufa maana nilikuja kugundua ya kuwa eneo la kichwa ndilo hutangulia, na maeneo mengine hufuatia kwa kuendelea kukomaa au kukauka au kujiunda na humalizikia mkiani. Sasa ukikimenya pale mwanzoni, unakifanya kife maana maeneo hayo mengine yanakuwa bado hayajafikia muda wake wa kukamilika.

Baya zaidi, yale mayai ambayo yameshaanza kumenyeka au kupasuka eneo la kichwa, niliyachukua baadhi (yaliyoelekea sana) na kuyapeleka eneo la kukuzia vifaranga. Hapo nikaja na kukuta vyote vimekufa kwa kuzidiwa na joto! Lo! Nikajifunza kitu. 

Kati ya funzo moja wapo la Kibaolojia ni kwamba, elimu ya kifizikia iliyotumika kutengeneza mashine ya kuatamieshia, imeundwa katika mfumo wa joto lililopangwa (mfano kwa vifaranga kwangu naweka 37.8) kuwa na uwezo wa kutoongezeka. Yaani halipandi kiasi cha kuadhiri mayai au vifaranga. Kwanza kuna feni na kuna hali ya unyevunyevu, pamoja na vifaa vilivyotumika kutokupata joto.

Nilipogusa sakafu ya eneo ambalo taa ya joto ipo, niligundua imekuwa na moto mkali sana. Mazingira ni ya joto mno. Nikagundua kuna kosa nimelifanya. Maana kwa vifaranga vilivyokwisha anguliwa, ni mazingira sahihi kabisa.

Katika maumivu ya kosa hilo, ndipo Roho Mtakatifu alipoingilia kati na kunifundisha somo la pili na lililokuwa muhimu sana kwangu. 

Ya kwamba, unashindwaje kuiamini "incubator" iliyokaa na yai siku 21 ya kwamba itakamilisha mchakato wote vizuri? (Nilipata ufahamu ya kwamba hapa kuna kosa ndani ya fikra na fahamu zangu.)

Kisha ukaja ujumbe ya kwamba, hata katika maisha ndivyo kwenye baadhi ya maeneo unashindwa kuniamini! Nikalazimika kuingia kwenye toba. Nikatubia hali ya kutokumuamini Roho Mtakatifu na kumtegemea; iwe ni katika huduma au maisha kwa ujumla wake. 

"Incubator" inawezaje kukuandalia kifaranga hadi kinachomoza kichwa, alafu wewe unafanya haraka na kutaka kikamilike kwa haraka zako! Mama anabeba mimba miezi 9 na kujifungua, alafu ashindwe kulea kweli? Sikatai kuna muda mfugaji unalazimika kukisaidia kifaranga kutoka kwenye kasha lake (hata kuku hufanya vivyo hivyo pia; ila ni baada ya kuwa na hakika kimekamilika

Kuna nafasi yetu katika maswala kadha wa kadha, ila kiuhalisia bado kuna namna ya kutenda na kuenenda pia. Taadhari hapa, isiwe katika hali ya kutokumuamini, kutilia shaka au kuwa na wasiwasi hali inayozaa tabia ya kutaka kumsaidia kazi au majukumu Roho Mtakatifu. Siku 21 zina kazi kubwa kuliko kifaranga kukauka katika kasha lake! 

Mungu anakuita, anakupa na karama sanjari na mwanzo mzuri wa kihuduma. Anakupa mahali pa kukanyaga na kadhalika, kisha unashindwa kumuani eneo la ujenzi wa jengo la kanisa ama ununuzi wa vyombo na hata ukuaji wa kanisa! Unaanza kulazimika kutumia akili na maarifa yako. Subiria kifaranga kikauke.

Usilazimishe huo uchumba, wala usilazimishe hiyo ndoa. Yai likikauka, tutajua kama ni la kuku au la chatu lilipenyezwa kwenye trei ya mayai ya kuku. Sasa ukilazimisha kabla ya wakati, ndipo unapojikuta unaingia ndani na unakuja kufahamu ulikosea kuoa au kuolewa. 

Lakini pia, kuna mayai niliyavunja na kugundua ndani bado kulikuwa na kifaranga ambacho kwa muda wake hakikuhitaji kupata hewa ya nje. Hivyo vilikufa, na niliyovivunja na kugundua mapema nililazimika kuziba kwa haraka; japo ni baadhi ndivyo nilivoviponyesha. Najua kwa wafugaji (muda uzidipo) hili ni la kawaida, ila hesabu zako za siku 21 zipo sawa? 

Epuka kulazimisha kuanza utumishi ama kufungua huduma, kufungua biashara kabla ya mazingira kukaa sawa. Kulazimisha mambo kumekuwa kukitugarimu sana katika maisha yetu. 

Somo hili lilinifanya kumwambia Mungu anisamehe kwa yale yote niliyowahi kuyalazimisha kwenye maisha na kuyaharibu au kuyadhoofisha. Lakini pia nikamtaka anisaidie kujifunza na kufaulu somo la kumuamini Yeye. Mfano, kuna ujenzi nilitaka kuuanza wa nyumba, nikawaza ni jenge jengo la muda la mafundi kuishi kwanza, na hata mimi pakufikia.

Nilipotulia, ndipo Roho Mtakatifu akanipa ufahamu moyoni, nami kujiuliza pamoja naye ya kuwa, gharama za ujenzi wa nyumba hiyo ya muda, na ile ya kudumu nizipige na kisha kuzilinganisha. Nikagundua zinanitosha kabisa kuanza sehemu ya awali ya nyumba nzima kwa kiwango cha zaidi ya nusu ya ujenzi. 

Nikaishilia kumshukuru Mungu, na kuwa na hitimisho zuri. Na hii ni faida ya kumshirikisha Roho Mtakatifu katika hali ya kumuamini yaani kumtumaini au kumtegemea kama nilivyokujuza katika Utangulizi wa Kitabu hiki na hata katika mada yetu ya pili ijayo. 

Kitabu Kikitoka Tafadhali Kitafute 

Kwa Vitabu km hivi Tuandikie Ujumbe wenye Neno VITABU Wasapu Nasi tutakutumia 

Namba Yetu +25559859287

Namba hizo zinaweza tumika kwa sadaka yako pia kupitia  M-Pesa, jina ni Oscar Samba.

Zaidi Endelea Kutembelea Sasa 

https://ukombozigospel.blogspot.com/?m=1 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni