Ujumbe huu ni Sehemu ya Kitabu Chetu Kipya cha; MOTO WA UAMSHO KATIKA BIBLIA
(Mwanzo Hadi Ufunuo.)
Na Mwalimu Oscar Samba
Utangulizi:
1.Kitabu hiki kimenuia kukusaidia kuona mbinu, kanuni, au matukio na matendo ya Kiungu ya kiuamsho katika Biblia.
2. Kina muwezesha Mkristo kwa muhubiri, kuisoma Biblia yote kwa sura ya kiuamsho.
3. Kinanuia kuibuisha tena kusudio la Kiungu lakuleta uamsho, au kuturejesha katika viwango vya kiroho.
4. Kinanuia kuunga mkono na kivitendo ajenda ya kanisa la nchi ya Tanzania na Afrika na baadhi ya makanisa ya nchi nyinginezo: inayohusu uamsho.
5. Ni muongozo wa Kibiblia wa kujifunza uamsho.
6. Itasaidia waalimu wa Biblia, au ibada zinazojifunza Biblia kama za Uanafunzi na maandiko, "Sunday School" na Bible Study.
Fahamu: Usomaji wa Biblia umekuwa ni chachu kubwa sana ulimwenguni na hususani katika historia ya kanisa; katika kuleta uamsho. Hata kipindi cha Agano la Kale, kuna tukio la mtu aliyekuwa akifanya usafi katika nyumba ya Bwana. Na alipokipata kitabu, akakitwa; kisha kikasomwa na watumishi wa Bwana mbele za watu: ndipo matengenezo makubwa yalipoibuka.
Uamsho wa Asusa, na mwingineo. Unachembembe kubwa za wanafunzi waliokuwa wakijifunza kwa pamoja. Na punde walipokifikia kitabu cha Matendo ya Mitume, ndipo walipojikuta wakilazimika kukisoma kwa msisitizo na upako wa utofauti sana. Mioyoni mwao kuliingia kiu ya kutaka kuiona Biblia inakuwa halisi kwao. Hususani katika eneo la ujazo wa nguvu na Roho Mtakatifu, pamoja na matendo yake kwao.
Hatuwezi kuutaka uamsho unaodumu, kama hatutajikita katika kuifahamu Biblia. Kuyafahamu maandiko. Kipimo, na kigezo chetu kikubwa cha uamsho ni lazima kiwe ni neno la Mungu. Lazima tujue sana kuwa, kuna aina fulani ya upako, au nguvu za Mungu; yaani moto wa Roho Mtakatifu ama muwako wake: uliopo katika neno lake.
Ndio maana, kati ya maeneo yenye upinzani mkubwa ni watu kusoma Biblia! Hata waombaji wengi na wana maombi: wana vifungo vikubwa, au ni wazito kusoma Biblia.
Na hata walio wepesi wa kuisoma, bado wengi wao wakiisoma ule uwezo wa kuielewa ni adimu sana kwao. Wengine ni wazito sio kuielewa tu, bali hawana utulivu wa kuisoma; na kuitafakari.
Tuna muda wakutosha kabisa kuangalia mpira, kutazama televisheni kama tamthilia, riwaya na maigizo mbali mbali; iila sio muda wa kusoma Biblia. Tuna utayari mkubwa kabisa wa kusoma magazeti na vitabu vya hadithi ila sio Biblia. Ni wepesi wa kupiga soga, na story mbalimbali ila ni wazito wa kuifungua Biblia. Tukisikiliza simulizi za kwenye redio hatukinai au "kuboeka" ila mahubiri yakizidi lisaa limoja ni kero kwetu! Miayo na malalamiko huibuka.
Muda wa kutazama runinga nyumbani hata watoto hawasinzii, ila ukisema tuombe kwa ajili ya kufungua ibada ya nyumba; hata anayeanzisha maombi anaanza kusinzia. Hadi aje aseme ameni; utashangaa na watu wazima walishaanza kuzama katika usingizi.
Huu ni usingizi wa kiroho. Kamwe tusipopigana nao, au kupambana nao; hatuwezi kupiga hatua kwenye eneo hili la kusoma maandiko. Mpenyo kwenye eneo la kusoma Biblia, lazima iwe ni kipaumbele chetu kikubwa. Vita hivi usipovishinda, ni vigumu kufikia malengo ya Kiroho.
Kitabu cha Matendo ya Mitume kipo wazi kabisa; ya kwamba wale ndugu walitulia katika fundisho la mitume. Watu wa Beroya walikuwa watulivu kiasi cha kuchunguza maandiko na kusoma kwa umakini mkubwa. Licha ya neno kuwa na dhima ya kumjua Mungu, na kuwasha Moto wa Umasho ndani yako, lakini pia neno ni Kinga dhidi ya imani potofu. Imani ambazo huzima au huchakachua sana moto wa Uamsho. Maana huo ni moto wa kigeni.
Karibu katika Kitabu hiki:
Kitabu cha Mwanzo:
Somo la 1: UKOMBOZI KWA MWANADAMU, Aliyeasi.
Na Mwl Oscar Samba
Neno kuasi hapa ni kwenda kinyume na maelekezo ya Mungu. Adamu na mkewe, walikubali kudaganywa na Shetani aliyemtumia mjumbe wake aitwaye nyoka; na hatimaye kumuasi Mungu. Katika hii mwanzo 2:17 Mungu anawaagiza wasile tunda husika. Na anamueleza Adamu wazi ya kuwa, siku wakila watakufa hakika.
Ni dhairi ya kuwa Adamu alishampa maelekezo hayo Hawa. Ambaye wakati wa maelekezo kutoka kwa Mungu moja kwa moja, alikuwa bado hajapewa mwili. Maana nyoka anavyoanza kumshawishi, inaonyesha kabisa alikuwa anaongea na mtu ambaye ameshataadharishwa.
Tazama; Mwanzo 3:1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?
Hatimaye mwanamke alikubali kudanganywa kwa hila za Shetani. Akatwa tunda akala, na kisha kumpa mumewe naye akala. Hapo mwanadamu akawa amekufa. Maana Mungu alishawaambia ya kuwa siku wakila watakufa hakika; Mwanzo 2:17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.
Licha ya kifo cha kimwili kilichokuja kudhiirika kwanza kwa Habili, na hata wao wawili kuja kufa; lakini pia kuna kifo cha kiroho. Ambapo kilimaanisha kutengwa na Mungu. Uhusiano wetu na Mungu kuvunjika.
Kumbuka katika uumbani Roho Mtakatifu anaonekana akiwa ametulia juu ya maji. Ikimaanisha makazi yake yalikuwa ni humu ulimwenguni. Lakini katika maisha ya watumishi wa Agano la Kale, tulikuwa tunamuona anawajilia watu kwa muda na kuondoka. Mfano kwa Samsoni na kadhalika. Hii ina maana kuwa dhambi iliharibu makao ya Uungu duaniani.
Hadi katika Agano Jipya, siku ya Pentekoste ndipo tunamuona akirejea tena. Na hapa wala hakai katika ulimwengu wote tena. Maana ulimwengu wote ulishamkataa katika bustani ile ya Edeni. Bali anakaa ndani ya waamini.
Sasa tutazame matukio ya Ukombozi huu:
1. Mungu Anamtafuta Mwanadamu Aliyepotea. Adamu na mkewe, mara baada ya kutenda dhambi walijificha. Dhambi iliwatenga na kuwaficha mbali na uso wake Mungu: lakini Mungu aliamua kuwatafuta na kuwarejesha tena katika wokovu.
Tazama; Mwanzo 3:9 BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? 10 Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.
Tukio hili, linafanana kabisa na hili la Zakayo. Ambapo hutudhiirishia dhima ya ukombozi hapa, ambayo ilikuja kukamilishwa na BWANA wetu Yesu Kristo; Luka 19:10 Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.
2. Aliachilia Mamlaka kwa Kanisa. Uzao wa mwanamke hapa unaliwakilisha kanisa, yaani wale tulio okoka; Mwanzo 3:15 nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.
Mamlaka hiyo, ndiyo hii hapa; Luka 10:17 Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. 18 Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. 19 Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.
Sio Mamlamka Dhidi ya Mapepo tu Bali na Magonjwa Pia: Mathayo 10:1 Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.
Mamlaka Katika Kila Jambo, la Duniani na la Ulimwengu wa Roho: Mathayo 16:18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.
19 Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.
3. Aliwapatia Wokovu. Hii ni ishara ya kusamehewa dhambi zao. Ni ishara ya kuwafufua kiroho. Wokovu ni kufufuliwa kutoka kwa wafu wa kiroho. Ni kuhuishwa tena kwa upya. Ni kuzaliwa mara ya pilia. Yohana 3:3-11.
Aliwashonea Vazi: Mungu aligundua watu hawa wamejishonea mavazi ya majani. Ambayo kiuhalisia hayawezi kuufunika mwili vizuri. Ndipo alipoona vyema kuwapatia vazi la ngozi. Ambalo lina uwezo mkubwa zaidi wa kuusitiri mwili.
Tazama; Mwanzo 3:21 BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.
Nasitwa fahamu vazi huwakilisha wokovu; Ufunuo wa Yohana 7:14 Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo.
Ufunuo wa Yohana 16:15 (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)
Vazi la Harusi Hapa Huwakilisha Wokovu; Mathayo 22:11 Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi.
Mathayo 22:12 Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. 13 Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Kifungu hicho kinatufundisha pia, kama huna vazi la Harusi, huwezi kuingia katika sherehe ya tukio husika. Vazi hukupa haki. Na ndivyo itakavyokuwa kwa watu wale ambao wanataka kuingia mbinguni lakini hawataki kuokoka.
Kumbuka uamsho wa kwanza kabisa ni wewe kuokoka. Kutubu dhambi, na kuyaishi maisha matakatifu. Maisha ambayo huwakilishwa na hayo maandiko ya Ufunuo wa Yohana hapo juu. Kuyafua maazi na kisha kuwa meupe ni ishara ya kutunza utakatifu. Kuna heri wenye hayo mavazi na kutunza; maana yake ipo baraka kwa wale wanaoutunza wokovu.
Kwa biyo, kuokoka ni jambo la kwanza. Au ni hatua ya awali, na kuutunza huo wokovu ni hatua nyingine kubwa na muhimu pia.
4. Aliwatakasa kwa Damu: Hapo anapoitaja Damu katika kuyafua hayo mavazi, inatujulisha wazi ya kuwa, katika mchakato wa wokovu huo, walisafishwa kwanza. Hiyo Ufunuo bapo juu inatuhakikishia ya kuwa damu ya Yesu ina dhima ya kuyafua mavazi. Kwa hiyo, inasafisha. Hakimisho la wazi tunalipata hapa; Waebrania 9:14 basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu/yaliyo kufa, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?
Sababu kubwa moja wapo tunayojulishwa hapo, ni kusafishwa ili wapate au tupate kumuabudu Mungu aliye hai. Maana kwa mujibu wa Mambo ya Walawi 17:11, kwenye damu kuna uhai. Mauti ya dhambi ya bustanini, inashindwa kwa huo uhai. Kwa hiyo, uchafu wa dhambi ni uwepo wa mauti ndani yetu. Tunasafishwa au walisafishwa ili kuondolewa mauti.
Hii ikupe kuhakikisha kama hujaokoka, unayesoma kitabu hiki unaokoka. Sijasema kama huna dini, au kama huendi kanisani, bali nimesema kama hujaokoka. Maana inawezekana unajiita mkristo lakini ndani yako hakuna ukristo; kuna mazoea na malezi tu ya kidini culani.
Ona tena hapa; 1 Yohana 1:7 bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
5. Damu ya Yesu Inadhima ya kurejesha Uhai. Na kama walivikwa ngozi ya mnyama pale bustanini; ni dhairi ya kuwa kuna mnyama alichinjwa. Na mnyama akichinjwa damu lazima imwagike. Kitu kilichokuwa kikiashirikia au kuwakilisha damu ya Yesu itakayokuja kumwagika msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Yaani kutufanyia ondoleo la dhambi.
Tazama; Mathayo 26:28 kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.
Oanisha na hili; 1 Wakorintho 5:7 Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo.
Tazama dhima ya hii Damu Katika Uhai: Mambo ya Walawi 17:11 Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi.
Kama ndivyo basi; damu ya Yesu imebeba uhai wa Yesu. Na kwa kuwa Yesu ni Mungu; uhai wa hiyo damu unakuwa ni uhai wa Kiungu. Na kilichotokea pale Edeni ni mauti, yaani uhai wa Kiungu kuondoka ndani yetu.
Sasa, ukiokoka; ni unarejeshewa huo uhai. Ndipo unapotimia ule msemo wa wanatheolojia unaosema ya kuwa; Adamu aliileta mauti katika mti wa uzima: lakini Yesu alileta uzima katika mti wa mauti. Warumi 5:19.
Nasi twafahamu dhairi ya kuwa; tafsiri au maana moja wapo ya uamsho ni kufufuka kutoka katika mauti. Kwa hiyo, unapookoka, ni unapokea hali ya kufufuka kutoka katika mauti ya dhambi. Na unapewa kuishi/uhai katika uzima wa Kiungu, kwa kupitia damu yake Yesu Kristo.
Hili inatupa kwanza kujitambua ya kuwa tulio okoka tumo ndani ya hatua ya mwanzo ya uamsho. Ambayo ni kuwa hai kwa jinsi ya mahusiano na Mungu. Yaani wokovu. Ambapo tunasalia na kazi moja ya kuitafuta hatua ya pili ambayo ni mmwagiko mkubwa wa nguvu za Mungu.
Huku ikimpa ole na ufunuo wa wazi yule ambaye hajaokoka na anatafuta hatua ya pili ambayo ni ya mmwagiko mkubwa wa nguvu za Mungu. Fahamu ya kuwa mahusiano na Mungu yana umuhimu mkubwa zaidi.
Lakini pia, Inapaswa Kutusukuma Katika Kuhakikisha Watu Wanaokolewa. Tunapo hubiri uamsho, tusijikite tu katika mmwagiko mkubwa wa nguvu za Mungu na kisha kutulia. Bali tujikite pia katika kuwafanya watu kuwa hai, hali itakayomwaga nguvu nyingi za Mungu ili kuwafufua kiroho. Na katika nguvu hizo, zile za ishara ya miujiza lazima zitakwepo tu.
Najua kati ya ugonjwa mkubwa kwa wapentekoste wa leo wanaousaka uamsho; ni kutokutafuta na kushika kanuni. Badala yake tunakimbizana na matokeo ya kanuni. Hii ni hatari.
6. Aliwafanyia Upatanisho. Kazi moja wapo kubwa ya damu, katika dhima ya mahusiano yetu na Mungu ni kufanya upatanisho. Dhambi iliwafarakaniha na Mungu. Kupitia mnyama aliyechinjwa kama sadaka, upatanisho uliweza kutokea. Ingawaje, iliendelea kusalia katika mfumo wa Agano la Kale. Ila ilikuwa ni utabiri au unabii wa upatanisho wa kudumu wa Agano Jipya.
Maana mnyama aliyechinjwa moja kwa moja alimwakilisha Yesu. Yesu alitufia akiwa hana hatia, asiyenakosa alikufa kwa ajili ya wenye kosa. Alikadhalika mnyama husika naye aliuawa kwa ajili yetu, sisi wenye kosa yaani wakina Adamu; tukapataniswa kwa sadaka ya damu ya mnyama ambaye hakufanya kosa hilo.
7. Alianzisha Mpango wa Mbingu Mpya na Nchi Mpya. Kitendo cha Mungu cha kuwafukuza, ili watoke katika bustani ya Edeni; kilikuwa cha upendo mkubwa sana. Kilijawa na upendo na mkakati mzuri wa ukombozi milele. Fahamu ya kuwa, kitu kilichowafanya kuondoshwa bustanini ni uwepo wa mti ambao tunda lake wakila wasingekufa tena milele.
Tazama; Mwanzo 3:22 BWANA Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele.
23 kwa hiyo BWANA Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.
Maana yake, kama wangekula; wasingekufa tena. Hii ina maana kwamba, mimi na wewe pamoja na wao, tungesalia katika ulimwengu huu wenye taabu na mwili huu wa mateso, na tamaa za dhambi milele na milele. (Tunda hili ni dawa ya kutibu kifo cha jinsi ya mwili tu, yaani huleta umilele katika maisha ya mwili. Halitibu kifo cha mahusiano kati ya Mungu na mtu. Ambapo hicho dawa yake ni wokovu. Na wangekula kabla kusingekuwa na madhara, maana tatizo lakubiwa halipo. Ndio maana haikuwa hatari kwao kabla ya kula tunda la ujuzi wa mema na mabaya. Lakini pia, lisingeweza kufanyika kinga maana halikuumbwa kwa namna hiyo. Suluhu lilikuwa ni kutii tu ie amri ya usile basi.)
Tuendelee: Kitu ambacho kingetuzuilia kufa. Na mtu aliyeo okoka, au kwa mtu aliyeo okoka kufa ni faida na sio hasara. Ni kifo pekee ambacho huweza kufanyika njia au mlango wa kuingia mbinguni.
Kuna maisha yanayoitwa ya Mbingu Mpya na Nchi Mpya. Huko ndiko mimi na wewe tuliye okoka tutaishi na Yesu milele na milele. Kwa sasa ukimuona Mungu utakufa, ila kipindi hicho makao au maskani ya Mungu yatakuwa pamoja nasi. Tutakuwa na furaha milele, maandiko hutuambia hakuna kuugua, magonjwa, huzuni wala machozi.
Yanafika mbali zaidi na kutueleza kuwa hakuna laana huko. Laana inayotajwa hapa ni ile ya bustani ya Edeni. Ya kwamba kwa jasho mtakula, utazaa kwa uchungu, aridhi itakuzalia miiba au michongoma na kadhalika. Hakikisha; Ufunuo wa Yohana 22:3 Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia.
Kumbuka, dhambi iliua uhusiano wetu na Mungu. Kwa hiyo, ikawa ni vigumu kumuona Mungu. Ni ngumu kuishi naye, Yesu akaja kama Imannueli yaani Mungu pamoja nasi. Ndio maana mara baada ya kifo na kufufuka kwake; Roho Mtakatifu akaja ndani yetu na pamoja yetu. Ikiwa ni mwendelezo wa dhima na dhana hii ya Mungu pamoja nasi. Ikinuia kufanya urejesho wa Edeni.
Sasa, utimilifu wa dhana hii ni katika Mbingu Mpya na nchi Mpya. Fahamu sana ya kuwa ina majina mawili au imegawanyika katika maeneo makuu mawili. Au ni muunganiko wa sehemu kuu mbili. Mosi ni mbingu, ambapo twafahamu ya kuwa ni makao au mkaazi ya Mungu. Pili ni nchi; ambapo kikawaida ni mkao ya mwanadamu. Au ni imaya ambayo mwandamu kapewa kuitawala. Kwa lugha nyingine ni dunia.
Kwa hiyo, Mbingu Mpya na Nchi Mpya huwakilisha maisha ya pamoja kati ya Mungu au Uungu, ama Ikulu ya mbinguni; ikiwakilisha na malaika zake, na kila kitu: pamoja na mwanadamu.
Tazama; Ufunuo wa Yohana 21:1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.
Ufunuo wa Yohana 21:2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.
3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.
5 Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.
6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.
Kwa hiyo, kama wasingefukuzawa, kisha wakatwa tunda wakala lile la kuishi milele na milele; maana yake na sisi tuliokuja kuzaliwa baada yao; tusingekufa. Na kama tusingekufa, tusingaliweza kuiridhi hii Mbingu Mpya na Nchi Mpya. Na umilele wa dunia hii ungetuhusu.
Na wala hatujapoteza kwa kupitwa na hili tunda; maana tunda hili tutakuja kulila huko mbinguni. Kwenye huo Mji wa Yerusalemu Mpya. Hakikisha; Ufunuo wa Yohana 2:7 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.
:2 katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.
7. Aliweka Uadui Kati Yetu (yao) na Shetani. Watu wengi hawajui ya kuwa kabla ya Mwanzo 3:15 Shetani hakuwa adui yetu. Hakuwa adui wa mwanadamu. Najua pia hakuwa rafiki wa mwanadamu pia. Alikuwa ni adui wa Mungu tu. Maana kule aliasi na alishakorifishana naye. Lakini kwa mwanadamu hakukwepo uadui wowote.
Ndio maana hata alipokwepo ndani ya nyoka, bado mwanadamu aliweza kuongea naye kama ada. Japo, kosa la mwanadamu lilikuwa ni kwenda kinyume na maagizo ya Mungu. Yaani kukosa utii. Lakini dhambi ilipoingia ulimwenguni, Mungu akaona sasa Shetani ni hatari kwa mwanadamu. Na akaweka uadui huo. Kwa hiyo, uadui baina yetu na Shetani umewekwa na Mungu mwenyewe.
Na sababu ni kwa sababu za uhatari wake kwetu. Lakini pia fahamu kama nyoka akiwa ni mnyama aliweza kulaaniwa (adhabu); maana yake alifahamu fika ya kuwa anachokifanya kinakwenda kinyume na agizo la Mungu. Na tunajulishwa ya kwamba, alipewa uwezo mkubwa wa ufahamu kuliko wanyama wote. Maandiko yakitumia neno uwerevu.
Kama angekuwa hajui, asingeadhibiwa. Na hii inaweza kuturudisha nyuma kabisa, kwenye kuyaona maisha kati yetu na wanyama kabla ya dhambi. Ni fika kuna uwezo wa utofauti wa kiufahamu walikuwa nao. Japo wengine wanaenda mbali zaidi na kusema yamkini wanyama nao walikuwa na uwezo wa kuongea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni