KURASA

Jumatatu, 17 Februari 2025

Mama Mchungaji: ISHINDE HOFU YA MAISHA YA BAADAE.


  Na Mwl Oscar Samba 

Ujumbe huu ni Sehemu ya Toleo la Pili la Kitabu Chetu cha NAFASI YA MAMA MCHUNGAJI; KATIKA HUDUMA YA MUMEWE.

Kwenye Pointi ya . Ishinde Hofu ya Kesho Kimkakati, (Maisha Baada ya Huduma au Uwepo wa Mume Wako). Kuna maisha baada au nje ya wito ama Utumishi. Umri ni kigezo muhimu cha kuweza kuwaondoa katika utumishi wa madhabahuni. Kifo pia ni njia ya jambo hili.

Ni kweli kabisa kumekwepo na maisha magumu, na hata manyanyaso mara baada ya mchungaji kufariki, kuondoshwa katika utumishi ama kustaafu. Mke na watoto au familia hujikuta wakiwa katika maisha yasiyo mepesi. Machozi ya uchungu na huzuni uwaandama. Malalmo na majeraha huwa sehemu ya maisha yao.

Hali hii imepelekea hofu kubwa katika nyumba nyingi za kitumishi. Watoto kwa mama wachungaji wamejikuta wakizungukwa na tatizo hili. Na hii

hutokana na kuitazama sadaka kama njia kuu ya kipato. Fikra hizi tunapaswa kuzishughulikia katika pointi hii. Tatizo hili lazima lipate tiba. Maana kama hii ndiyo njia pekee, ni nini kitatokea kama leo mume wako atapokonywa kanisa! Haijalishi ni kwa haki au kwa kuonewa! Nini kitatokea kama Mungu akimuita mbinguni mume wako?

Sijui madhehebu mengine, ila langu katika katiba yake limetamka bayana ya kuwa kama mume au mke akifariki ambaye ndiye aliyekuwa mchungaji hapo, mwenza wake hata kama ni mchungaji au mtoto; hawezi kurithishwa hilo kanisa. Sina shida hata chembe na utaratibu huu, maana ni Kibiblia na ni wa dhati kabisa.

Ni hatari tukayafanya makanisa kuwa ni mali ya uridhi. Kuna siku kikao cha miradhi ya familia kitakaa na  kuanza kutafuta mridhi wa kanisa au huduma. Lazima tuwe na mipango ya kulinusuru hili. Hata wake wasio kuwa na wito nao watajipenyeza humu, watoto na wanafamilia ambao yamkini hata kiroho chao hakijakaa sawa wanaweza kuutumia mwanya huu. Hali ambayo itawapeleka pabaya sana.

Sasa, chakufanya ni kuhakikisha ya kuwa unakuwa na mipango dhabiti; wewe na mumeo ya uwekezaji wa kimaisha, kwa ajili ya maisha yenu ya sasa na baadae. Fahamu pointi hii inagusia kuishinda hofu ya namna hii kimkakati. Nayanena haya maana kuna watu wanalazimika kuhama katika makanisa au madhehebu yenye kanuni kama hizi; ya kwamba mke au mtoto wa marehemu hawezi kurithishwa kanisa; kutokana tu na hofu hii.

Maana familia imeshalitazama kanisa kama sehemu ya kipato. Na wengine wanagoma au wanakuwa wazito kustaafu kwa hofu kama hizi. Lakini pia wapo ambao hata wakistaafu bado wanataka waendelee kupewa posho. Ndiposa wengine wanatafuta mtu wakukaa hapo kanisani, au wakumfanya kuwa mchungaji ili tu ahakikishe anampatia posho! Yaani mtu wa kumlinda.

Mkakati wa kwanza ni kumshauri mume wako, kuweka akiba kidogokidogo katika mfumo wa mafao wa uzeeni. Kwenye dhehebu langu mfuko huu upo, unaitwa TPPF, ambapo kila asilimia 5, huwa inaingia huko, ya pato la kila mwezi. Hata kama kwako haupo, unaweza kujiunga na mfuko wa madhehebu mengine. Au hata mifuko ile ya kiserikali  ama mingineyo kama NSSF. 

Pia, mnapaswa kuwa na "akaunti" maalumu ya fedha ya benki. Benki kadhaa zina utaratibu wa kuwa na akaunti hizo maalumu kwa ajili ya akiba. Ambapo huruhusiwi kutoa fedha kila wakati, kunakuwa na muda au sababu maalumu za kufanya hivyo. Kumbuka waswahili husema ya kuwa akiba haiozi. 

Wekezeni. Siwezi kukupangia mahali pa kuwekeza, ila sio vyema pia mama mchungaji akaa tu bila chakufanya. Najua inategemea na mazingira ya kihuduma, lakini hata kama mmefanikiwa au kutingwa kihuduma kiasi gani; bado kuna aina ya miradi anaweza kupaswa kuisimamia. Mume akiondoka leo, walau una uzoefu wa kuuza nyanya, au mkaa. Genge la bamia na kibanda cha vitumbua havikushindi.

Ushauri wangu mkubwa hapa ni katika aina ya miradi ambayo haitadhiri kiroho chenu. Lakini pia ambayo haiwezi kuadhiri muda wenu na Mungu. Kwa Mungu huduma ni kipaumbele kikubwa zaidi, kuliko fedha. Kwake mkikorofisha hapo, ni bora mkaishi kama ndege; lakini kazi yake iende. Kitabu kile cha UTUMISHI NA FEDHA kitakusaidia sana ili muweze kuwa salama hapa.

Uwekezaji kama wa nyumba ya kupangisha ni muhimu sana kwenu. Mkiweza ziwe nyingi. Maana usimamizi wake ni mdogo, hauwezi kuwaadhiri kivyovyote vile. Na nyumba haiozi wala haiwezi kuibiwa. Hata kukitokea mdororo wa uchumi, haiwezi kukata mtaji. 

Mfano mimi kwa sasa nimewekeza kwenye kilimo cha kulima mpunga. Na wewe tazama kwenye eneo lako ni fursa ipi inayoweza kutumika vyema na ikakuongezea kipato. Fahamu ya kuwa hapa lengo ni kuishinda hofu ya baadae. Sasa huna budi kuhakikisha ya kwamba, faida ya kila uwekezaji inaingia katika uwezaji mwingine wa kudumu zaidi. Uwe na kitu ambacho hata ukifa unaweza warithisha watoto wako. Mashamba ni kimoja wapo. Biashara endelevu na kadhalika.

Najua uwekezaji ni vita. Kwa hiyo, ukiona mipango yako ya kuwekeza ni migumu uwe na hakika ni aina ya vita. Lazima uvishinde. Adui akijua huna hofu ya unga nyumbani, huna mashaka na kesho yako hususani wewe na familia yako; anafahamu ni umempiga chenga kubwa sana ya kiutumishi.

Wekeza Katika Elimu ya Watoto Wako. Ni muhimu kupambana kadri uwezavyo ili kuwajengea wanao msingi bora wa kielimu, msingi ambao ni muhimu sana kwao. Imani ya kuwa Mungu anashughulika sana na mambo yetu, haipaswi kutumika kama njia ya sisi kushindwa kujitahidi kuijenga misingi mizuri kwao. Hayo ni matumizi mbaya sio ya imani tu bali hata maandiko.

Lazima tuepuke utamaduni wa kulazimisha au wakutaka familia zetu nazo ziwe na utumishi. Wewe ukiitwa, siilazima na mtoto au mwanao naye aitwe. Kwa hiyo, fikra za ya kwamba akiwa mkubwa atatumika kama mimi au kama baba yake; zikikosekana: zitakusukuma kumpatia elimu bora. Na hata kama kaitwa kweli, bado Mungu anahitaji wasomi pia, kama wakina Tabibu Luka walivyofanya kazi kipindi kile cha kanisa la kwanza sanjari pia na Paulo Mtume. Ambaye usomi wake ulilisaidia sana kanisa hata sasa.

Nakutaka kulitambua hili ili ukuze karama au kipaji ambacho Mungu ameweka ndani ya wanao, na sio wewe utengeneze kipawa au wito ndani yake na kulazimisha kuupalilia. Hili ni kosa sana. Mafanikio ya mtu yamefungwa katika zawadi au kipawa alichopewa na Mungu. Tazama Mithali ... (Mithali 17:8 Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa.)

Hutuambia kila kinapogeuka ndipo hufanikiwa. Hasemi wito bali ni kile alichopewa mtu na Mungu. (Watumishi wengi wamekuwa wakiwaita watoto wao!)

Kufanikiwa kwa wanao baadae ni kufanikiwa kwenu pia, ni baraka sana watoto wa watumishi kufanikiwa kimaisha. Maana watakuwa ni sehemu ya kuibariki familia yote. Na hofu ya kesho unakuwa umeishinda; kwao kwenu.

Nidhamu katika fedha. Fedha ni jambo linalohitaji nidhamu kubwa sana. Usiiweke imani kila mahali, imani ikikaa eneo ambalo sio sahihi inakuwa sio imani bali ni ujinga wa kifikra. Mfano mama mchungaji mmoja aliwahi kuhitaji fedha kwa mtu, na yule mtu akamwambia hii nimeiweka niitumie kesho kutwa katika jambo fulani. Akamtia moyo waitumie muda ule, huku akimwambia kuwa; kwani huna imani ya kwamba Mungu atakuwa ameshakupa fedha nyingine hadi wakati huo!

Msile kila fedha kama mchwa. Hata mchwa na chungu au sisimizi huwa wana utamaduni wa kijiwekea akiba. Lazima muwe na tabia ya kuhakikisha kila fedha inayopita katika mikono yenu mnaitumia kiusahihi.

Tumbo haliridhiki, na halijawahi kuridhika. Tena ukiliendekeza sana litaishia kukuzalia kisukari na shindikizo la damu. Pia maisha ya anasa sio salama. Lazima ujifunze kupunguza matumizi yasiyo sahihi, kujibana nayo ni kiroho. Mtume Paulo analisisitiza hili. 

Tazama; Tito 3:14 Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda. 

Unaposhindwa kuwa na kipaumbele, au kuelekeza matumizi ya fedha zako katika mambo ya lazima ni unajizuia kuwa na matunda. Kuwa na mafanikio katika fedha inayopita mikononi mwenu ni swala muhimu sana. Kama huna uwakika na kesho yako, au wanao hawana. Ni dhairi wataingiwa na hali ya hofu kuihusu. Hofu ambayo kivyovyote vile itawafanya kulitazama kanisa kama fao la uzeeni. Na kama kuhimili au uti wa mgongo wa uchumi wenu. Na nguzo ya kati katika zile nyumba zenye nguzo moja ya katikati tu: huwa inalindwa sana!

Muwe na Vipaumbele. Lazima muhakikishe mna vipaumbele vya uwekezaji. Maandiko husema ya kuwa, pasipo maono hakuna kujizuia. Mbele yake anaitaja sheria...( Mithali 29:18 Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria. Where there is no vision, the people perish: but he that keepeth the law, happy is he.)

Kwa maana kwamba, kama hamna vipaumbele ni dhairi kuwa, kila fedha itakayokuwa inapita mikononi mwenu huishilia katika matumizi yoyote yale. Na ukijiona ya kuwa, kabati la nguo ni kubwa kuliko mipango mliyo nayo kama familia; ni umeifuata njia yenye kulitazama kanisa kama uti wa mgongo wa uchumi wenu: sasa na baadae. Jambo ambalo ni hatari sana. Ukiona pia friji au chombo cha kuweka akiba ya chakula kisioze ni kikubwa kuliko malengo ya uwekezaji mliyo nayo; ni mmeifuata njia isiyokuwa na matumaini. Maana kila unachokula huwa kinaoza, ila uwekezaji hauozi.

Kuwa na nyumba ya kuishi ni sehemu muhimu ya kuwekea kipaumbele, ili hata mumeo akilala leo au utumishi ukikwama, tayari hamdaiwi kodi. Hamuwezi kukimbia mjini ama kunyanyasika kisa mmeishiwa kodi! Fahamu sana ya kuwa, asiye na malengo au maono ni sawa na kipofu au mtu aliyekosa macho. Kukosa vipaumbele vya kimaendeleo ni sawa na kuamua kuiendea njia yoyote ile; na utafika popote. 

Kitabu Kikitoka Kitafute:

Mawasiliano:

Tutembele ama Wasiliana Nasi 


http://www.ukombozigospel.blogspot.com


Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo; 


https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h


Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD


Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk


Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv


Kwa Maombi +255759859287, Email: ukombozigospel@gmail.com


Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook: 


https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbWKwL


Tuandikie pia Maoni Yako; mwalimuoscarvitabu@gmail.com


Kava;

Kitabu Hiki Kina Manufaa Pia Kwa Wake za Viongozi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni