KURASA

Alhamisi, 13 Februari 2025

CHUNGA MNASEMA NINI MBELE YA FAMILIA NA WASHIRIKA.


Ujumbe huu ni Sehemu ya Kitabu cha NAFASI YA MAMA MCHUNGAJI; KATIKA HUDUMA YA MUMEWE, Toleo la Pili.

Na Mwalimu Oscar Samba
Katika hii pointi ya Chunga Mnasema Nini Mbele ya Familia, Uzao Wako, Washirika au Kanisa Kuhusu Dhehebu, Viongozi Wako wa Kiroho Dhidi ya Wito Wenu au Utumishi.

Unachopanda Kinaota. Linda Sana Unapanda nini katika fikra na mioyo yao. Watoto ndio kanisa la sasa na kesho. Washirika ndio watumishi wanaoandaliwa. Unaandaa watumishi wa aina gani?

Kumbuka, Upandacho Ndicho Uvunacho. Au Upandacho, Ndicho Tuvunacho!
Iwe ni wewe au mmeo, ama mtumishi mwingine katika madhabahu mliyopewa na Bwana, huna budi kuhakikisha udhaifu huo unaondoka miongoni mwenu. Mbegu nyingi za uasi zinapandwa mioyoni mwa washirika, au watoto kama sehemu ya manung'uniko kutoka kwa wazazi au watumishi wao. Wataponda dhehebu lao, watachambua kila madhaifu, lakini wao hawatoki; wanakuja kushangaa baadae wana watoto au washirika wasiopenda dhehbu la wazazi wao! Wanaanza kutafuta na kujaribu kuwarudisha bila mafanikio!

Hakuna sehemu isiyokuwa na madhaifu, hakuna viongozi waliokamilika. Sema tu, unafanya nini kukabiliana na hayo madhaifu ya wengine hapo ndipo swali lilipo. Malalamiko ya kwamba katika dini hii mchungaji binafsi huwezi kuendelea, michango ni mingi, mara mimi mchungaji nikifa leo mke wangu hatathaminiwa, ni miongoni mwa mambo ya kulinda sana. Mioyo ya watoto huumia wanaposhirikishwa maumivu ya wazazi, na tena huumia zaidi. Wanaanza kukua na "mentality" ya kwamba dini hii inawanyanyasa wazazi wangu. Fikra hizi zinakuja kuamia kwenye mioyo yao.

Machozi unayolizwa na viongozi yalilie bafuni, ili ukimaliza kulia maji unayoogea yaweze kuyasafirisha machozi yote; na lisisalie hata moja. Daudi hakuruhusu ubaya wa Sauli mfalme kuendelea kwenye moyo wa Sulemani mwanaye. Lazima hekima ya namna hii tuwe nayo. Ni hatari tukampa adui Shetani nafasi ya kutufanya kuandaa kizazi chenye "elements" au chembechembe za uasi ndani yake. Na uasi unaotokana na maumivu ni mbaya sana. Magumu unayoyapitia mengine umeandikiwa na Mungu ili baadae ukijakuwa kiongozi uweze kuja kuwa mtu sahihi kwa watu wako.

Nimeshuhudia mtoto wa mchungaji mmoja toka akiwa shule ya msingi na kisha sekondari akijisemea ya kuwa: siku nikiwa mkubwa sitafungua kanisa TAG, Kisa maneno ya malalamiko kutoka kwa wazazi wake. Wenzangu niliokuwa nao wengi walihama dini, kisa mbegu kama hizi. Baadae wanakuja kugundua ya kuwa walifanya maamuzi yasiyo sahihi!

Chunga sana, unalalamika nini kuhusu dhehebu, viongozi wako wa kidini, au utumishi ulio nao mbele ya watoto, uzao wako, mwenza wako na hata kanisa kwa ujumla! Kile unachokifanya kinapandwa ndani yao kama mbegu. Kuotesha mchongoma ni kazi ndogo sana, ila kuung'oa ni kubwa mno.

Baya zaidi, wengine wanachambua madhaifu kama haya, hata mbele ya watumishi ambao wapo chini yao, au ambao tayari anawaanda kabisa kuwa watumishi. Hili ni tatizo kubwa sana. Ni sawa na kubandua vipande vya boti vilivyowekwa kwenye nyufa au maungio ya mbao ya boti mliyoipanda.

Muungwana hutafuta na gundi ili kuziba vizuri kwa nia ya kupaimarisha zaidi. Ni lazima fikra zetu zifikie mahali pa kukua na kukomaa vizuri kabisa katika hili.

Kitabu Kikitoka Kitafute:
Mawasiliano:
Tutembele ama Wasiliana Nasi

http://www.ukombozigospel.blogspot.com

Tumeunda Channel ya WhatApp, Tufolo;

https://whatsapp.com/channel/0029Va827LBJENy9u6Enke1h

Kundi letu la WhatsApp https://chat.whatsapp.com/E0eD0xegh1eIGMjRykPyRD

Telegram https://t.me/+fft3GHXC9xIzYjhk

Subscribe YouTube yetu: https://www.youtube.com/@ukombozigospeltv

Kwa Maombi +255759859287, Email: ukombozigospel@gmail.com

Usiache Kutembelea na Ku-Like Page Yetu Ya Mafundisho ya Neno la Mungu Facebook:

https://www.facebook.com/MafundishoyanenolaMungunamwalimuoscarsamba?mibextid=ZbW

KwL

Tuandikie pia Maoni Yako; mwalimuoscarvitabu@gmail.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni